Back to Swahili New Testament Bible online homepage (Contents Page of Online Bible)
1 Corinthians 14 [1]
[2]
[3]
[4]
[5]
[6]
[7]
[8]
[9]
[10]
[11]
[12]
[13]
[14]
[15]
[16]
1COR 14:1 Jitahidini kuwa na upendo. Vilevile fanyeni bidii ya kupata vipaji vingine vya kiroho, hasa kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu.
1COR 14:2 Mwenye kunena lugha ngeni hasemi na watu bali anasema na Mungu. Yeye hunena kwa nguvu ya Roho mambo yaliyofichika.
1COR 14:3 Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, husema na watu kwa ajili ya kuwajenga, kuwafariji na kuwatia moyo.
1COR 14:4 Mwenye kunena lugha ngeni anajijenga mwenyewe. Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, analijenga kanisa.
1COR 14:5 Basi, ningependa ninyi nyote mseme kwa lugha ngeni lakini ningependelea hasa muwe na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, maana mtu mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, ni wa maana zaidi kuliko yule mwenye kusema lugha ngeni, isipokuwa tu kama yupo hapo mtu awezaye kuyafafanua hayo mambo asemayo, ili kanisa lipate kujengwa.
1COR 14:6 Hivyo, ndugu zangu, kama nikija kwenu na kusema nanyi kwa lugha ngeni itawafaa nini? Haitawafaa chochote, isipokuwa tu kama nitawaelezeni ufunuo wa Mungu au ujuzi fulani au ujumbe wa Mungu au mafundisho fulani.
1COR 14:7 Ndivyo ilivyo kwa vyombo visivyo na uhai vyenye kutoa sauti kama vile filimbi au kinanda. Je, mtu anawezaje kuutambua wimbo unaochezwa kama vyombo hivyo havitoi sauti waziwazi vinapopigwa?
1COR 14:8 La mgambo likilia bila kufuata taratibu zake, nani atajiweka tayari kwa vita?
1COR 14:9 Hali kadhalika na ninyi, kama ulimi wenu hausemi kitu chenye kueleweka, nani ataweza kufahamu mnayosema? Maneno yenu yatapotea hewani.
1COR 14:10 Zipo lugha mbalimbali ulimwenguni, na hakuna hata mojawapo isiyo na maana.
1COR 14:11 Lakini ikiwa mimi sifahamu maana ya lugha asemayo mtu fulani, mimi ni mgeni kwake mtu huyo naye pia ni mgeni kwangu.
1COR 14:12 Hali kadhalika na ninyi, maadam mna hamu ya kupata vipaji vya Roho, jitahidini hasa kujipatia vile vinavyosaidia kulijenga kanisa.
1COR 14:13 Kwa hiyo, mwenye kunena lugha ngeni na aombe apate uwezo wa kuzifafanua.
1COR 14:14 Maana, nikisali kwa lugha ngeni roho yangu ndiyo inayosali, lakini akili yangu hubaki bure.
1COR 14:15 Nifanye nini, basi? Nitasali kwa roho yangu, nitasali pia kwa akili yangu; nitaimba kwa roho yangu, nitaimba pia kwa akili yangu.
1COR 14:16 Ukimsifu Mungu kwa roho yako tu, atawezaje mtu wa kawaida aliye katika mkutano kuitikia sala yako ya shukrani kwa kusema: "Amina," kama haelewi unachosema?
1COR 14:17 Sala yako ya shukrani yaweza kweli kuwa bora, lakini huyo mwingine haitamfaidia.
1COR 14:18 Namshukuru Mungu kwamba mimi nasema kwa lugha ngeni zaidi kuliko ninyi nyote.
1COR 14:19 Lakini katika mikutano ya waumini napendelea zaidi kusema maneno matano yenye kueleweka ili niwafundishe wengine, kuliko kusema maneno elfu ya lugha ngeni.
1COR 14:20 Ndugu, msiwe kama watoto katika fikira zenu. Kuhusu uovu muwe kama watoto wachanga lakini katika kufikiri ni lazima muwe kama watu waliokomaa.
1COR 14:21 Imeandikwa katika Sheria: "Bwana asema hivi: `Kwa njia ya wenye kunena lugha ngeni, na kwa midomo ya wageni, nitasema na watu hawa, hata hivyo, hawatanisikiliza."`
1COR 14:22 Hivyo basi, kipaji cha kusema lugha ngeni ni ishara, si kwa ajili ya watu wenye imani, bali kwa ajili ya wale wasioamini; lakini kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni kwa ajili ya wale wanaoamini na si kwa ajili ya wasioamini.
1COR 14:23 Basi, kanisa lote linapokutana pamoja, na wote wakaanza kusema kwa lugha ngeni, kama wakija watu wa kawaida au wasioamini, je, hawatasema kwamba ninyi mna wazimu?
1COR 14:24 Lakini, wote wakiwa wanautangaza ujumbe wa Mungu, akija mtu wa kawaida au asiyeamini, yote atakayosikia yatamhakikishia ubaya wake mwenyewe; yote atakayosikia yatamhukumu.
1COR 14:25 Siri za moyo wake zitafichuliwa, naye atapiga magoti na kumwabudu Mungu akisema: "Kweli Mungu yupo pamoja nanyi."
1COR 14:26 Ndugu, tuseme nini, basi? Mnapokutana pamoja, mmoja aimbe wimbo, mwingine atoe mafundisho, mwingine awe na ufunuo kutoka kwa Mungu, mwingine atumie kipaji cha kusema kwa lugha ngeni na mwingine afafanue yanayosemwa. Yote yawe kwa ajili ya kulijenga kanisa.
1COR 14:27 Wakiwepo watu wenye vipaji vya kusema kwa lugha ngeni, waseme wawili au watatu, si zaidi, tena mmojammoja; na aweko mtu wa kufafanua yanayosemwa.
1COR 14:28 Lakini kama hakuna awezaye kufafanua, basi, mwenye kusema lugha ngeni anyamaze mkutanoni, aseme na nafsi yake mwenyewe na Mungu.
1COR 14:29 Kuhusu wale wenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, waseme wawili au watatu, na wengine wayapime maneno yao.
1COR 14:30 Ikiwa mmoja anaposema mwingine wa wasikilizaji amepata ufunuo kutoka kwa Mungu, basi, yule anayesema anyamaze.
1COR 14:31 Maana nyote mwaweza kutangaza ujumbe wa Mungu, mmoja baada ya mwingine, ili nyote mpate kujifunza na kutiwa moyo.
1COR 14:32 Kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni lazima kitawaliwe na huyo mwenye hicho kipaji.
1COR 14:33 Maana Mungu si Mungu wa fujo, ila wa amani.
1COR 14:34 Kama ilivyo desturi katika makanisa yote ya watu wa Mungu, wanawake wakae kimya katika mikutano ya waumini. Hawana ruhusa kusema; ila wawe watii kama isemavyo Sheria.
1COR 14:35 Ikiwa wanayo maswali ya kuuliza, wawaulize waume zao nyumbani, maana ni aibu kwa mwanamke kusema katika mikutano ya waumini.
1COR 14:36 Je, mnadhani neno la Mungu limetoka kwenu ninyi au kwamba limewajieni ninyi peke yenu?
1COR 14:37 Kama mtu yeyote anadhani kwamba yeye ni mjumbe wa Mungu au kwamba anacho kipaji cha Roho, na ajue kwamba haya ninayowaandikia ninyi ni amri ya Bwana.
1COR 14:38 Lakini mtu asiyetambua hayo, basi, mtu asimjali mtu huyo.
1COR 14:39 Hivyo basi, ndugu zangu, mnapaswa kuwa na hamu ya kutangaza ujumbe wa Mungu; lakini msimkataze mtu kusema kwa lugha ngeni.
1COR 14:40 Lakini yote yafanyike kwa heshima na kwa utaratibu.
Search the online bible
Back to Jesus Work Ministry main home page
Back to Jesus Work Ministry home for spiritual warfare and Christian deliverance ministry
Back to Jesus Work Ministry home for resources on Christian living
Christian deliverance and Spiritual warfare book 1
Christian deliverance and Spiritual warfare book 2
Christian deliverance and Spiritual warfare book 3
Christian deliverance and Spiritual warfare book 4
Spiritual warfare and Christian deliverance ministry classics
Other spiritual warfare and Christian deliverance resources on Jesus Work Ministry
Christian deliverance and spiritual warfare audio sermons (free Christian MP3 audio downloads)